TFS haijazuia vibali vya kukamilisha miradi ya umeme vijijini

0
198

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja amesema, serikali kupitia Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), haijazuia vibali vya kukamilisha miradi ya kimkakati ya kupeleka umeme vijijini kwa kupitisha nguzo za umeme katika hifadhi za misitu nchini.

Ameyasema hayo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msambatavangu aliyetaka kujua mikakati ya Serikali ya kutochelewesha vibali vya kuruhusu umeme kupita kwenye hifadhi za misitu ili kuwahisha usambazaji wa umeme vijijini.

“Sheria ya Misitu Sura ya 323 haijazuia upitishaji wa nguzo za umeme katika Hifadhi za Misitu hapa nchini” amesisitiza Masanja

Amefafanua kuwa Kifungu cha 26 cha Sheria ya Misitu Na. 14 ya mwaka 2002, kimeweka utaratibu kwa taasisi/mtu anayetaka kufanya shughuli mbalimbali ndani ya Hifadhi ya Msitu na utaratibu huo unamtaka mtu huyo au taasisi kuwa na kibali kutoka kwa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kinachomruhusu kufanya shughuli husika.

Aidha, Naibu waziri huyo wa Maliasili na Utalii ameeleza kuwa Serikali kupitia TFS kwa nyakati tofauti imekuwa ikizishirikisha Wizara za kisekta kukamilisha miradi ya kimkakati ya kupeleka umeme vijijini bila kuchelewa.