TFF yamwachia huru Mwakalebela, kocha afungiwa maisha

0
238

Makamu Mwenyekiti wa klabu ya Yanga, Fredrick Mwakalebela ameondolewa adhabu ya kutojihusisha na soka kwa miaka mitano (ndani na nje ya Tanzania) na faini ya shilingi milioni 7 baada ya kushinda kesi mbele ya Kamati ya Maadili ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF).

Mwakalebela amekiri na kusema anajutia kosa na kuomba aondolewe adhabu hiyo ambayo tayari ameitii kwa kipindi cha miezi miwili.

Mbele ya Kamati hiyo ya Maadili ya TFF, Mwakalebela aliomba apewe fursa nyingine ya kuutumikia mpira wa miguu na kuahidi kuwa muadilifu kwa kufuata na kuheshimu sheria na kanuni zinazotawala mpira wa miguu.

Mwanasoka huyo alipewa adhabu hiyo Aprili 2 mwaka huu, kwa madai mbalimbali ikiwemo kutoa taarifa za uongo kuwa TFF inaihujumu Yanga.

Mbali na Mwakalebela, kamati hiyo pia imekubali maombi ya marejeo ya Wanachama wawili wa Yanga, Bakili Makele na Boazi Ikupilika kufutiwa adhabu ya kufungiwa miaka mitatu kila mmoja kwa kupinga kwa makusudi maelekezo ya Baraza la Michezo la Taifa (BMT) ya namana ya kufanyika uchaguzi wa klabu ya Yanga iliyotolewa na kamati mwaka 2018.

Katika hatua nyingine Kamati ya Maadili ya TFF imemfungia maisha kocha Liston Katabazi kujihusisha na mpira wa miguu ndani na nje ya Tanzania kwa kutoa shutuma za uongo dhidi ya TFF ambazo alishindwa kuthibitisha.