TEITI yashiriki Maonesho ya 45 ya Sabasaba, yatoa elimu kwa wananchi

0
182

Taasisi ya uhamasishaji uwazi na uwajibikaji katika rasilimali madini,mafuta na gesi asilia Tanzania–TEITI imesema mafanikio makubwa yameanza kuonekana katika sekta ya Madini, Mafuta na Gesi Asilia hapa nchini kutokana na kuwepo kwa uwazi katika uendeshaji wa shughuli hizo hapa nchni.

Hivi karibuni TEITI imeweka wazi kwa umma Ripoti yake ya 11 kwa mwaka 2018/2019 ambayo inaonesha kuwa uwazi katika sekta hizo unazidi kuonekana ambapo kila upande unafahamu kuhusiana na malipo na mapato yanayotokana na shughuli za utafutaji na uchimbaji wa Madini, Gesi na Mafuta.

Afisa usimamizi wa Fedha kutoka TEITI -Bw.Erick Ketagory amesema, katika ripoti ya mwaka 2018/2019 serikali imeripoti kupokea kiasi cha Tshs shilingi Bilioni 623 kutoka kwa makampuni yaliyofanyiwa ulinganishi na Tshs bilioni 626 zimeripotiwa kulipwa na Makampuni hayo na kupelekea tofauti ya Tshs bilioni 2.9 kati ya Malipo na mapato ya serikali.

Ketagory amesema, TEITI inaendelea kutoa elimu kuhusiana na uendeshaji wa uwazi na uwajibikaji katika sekta hizo na wameamua kushiriki Maonesho ya Sabasaba ili kuendelea kutoa elimu kwa wananchi wanaotembelea banda lao.

Aidha, Ketagory ametoa rai kwa wananchi kutembelea banda la TEITI lililopo ndani ya banda la Wizara ya Madini ili wapate elimu na kuifahamu taasisi hiyo inayosimamia uwazi na uwajibikaji katika rasilimali madini,mafuta na gesi asilia.