TEHAMA kuipaisha Tanzania Kimataifa

0
141

Serikali imewataka wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini, kuifikisha nchi ya Tanzania kwenye ngazi inayostahili, ili kwenda sambamba na ukuaji na mabadiliko ya TEHAMA nchini.

Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Jim Yonazi wakati akifungua kikao cha kutathmini mahitaji ya taaluma ya TEHAMA nchini kilichofanyika jijini Arusha, ambapo kikao hicho kimewakutanisha Wakurugenzi wa TEHAMA na Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimali Watu wa Wizara zote nchini ili kwa pamoja waweze kujadiliana na kuibua mahitaji ya taaluma hiyo Serikalini.

“Wakurugenzi mliopo hapa ni vema mtambue vipaji na kuviendeleza kwa kuwa dunia imebadilika, tuwatumie watumishi waliopo Serikalini na kuwaendeleza ili wafikishe nchi tunapohitaji na kuhakikisha wanakuwa wabunifu,” amesisitiza Dkt. Yonazi

Amesema kuwa Wizara imepewa dhamana ya kusimamia TEHAMA nchini, hivyo utekelezaji wa majukumu yao mahali pa kazi lazima TEHAMA itumike kwa maendeleo ya taifa kwa kuwa Serikali inatumia TEHAMA kuhudumia wananchi; wananchi wanawasiliana baina yao; inarahisisha shughuli za kiuchumi, kijamii na utawala; na inatumika katika kutoa na kupata huduma mbali mbali bila mtu kulazimika kusafiri kama vile kupata huduma za kibenki; kulipia maji, umeme, bima, leseni; huduma mtandao za afya, elimu

Akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi wa TEHAMA wa Wizara hiyo, Mulembwa Munaku amesema kuwa mafunzo haya yatatolewa kwa wataalam wa TEHAMA 500 na wataalam wa kada nyingine ili kuhakikisha kuwa watumishi wa umma wanapatiwa mafunzo ya msingi ya TEHAMA kwa kuwa wakati mwingine unakuta kompyuta tu imezimika ila mtumishi haelewi namna ya kuiwasha, hivyo ni muhimu kutoa mafunzo kwa watumishi wa umma