TCU yapunguza siku za uhakiki wa vyeti vya wanafunzi

0
416

Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) katika kipindi cha mwezi Novemba 2015 hadi Novemba 2019 imefanya uhakiki na utambuzi wa uhalali wa vyeti 8,328 vya wahitimu waliotunukiwa tuzo zao na vyuo vikuu vilivyo nje ya Tanzania.

Katibu Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa alisema kutokana na kuimarika kwa mifumo ya kieletroniki, TCU imefanikiwa kupunguza muda wa uhakiki na utambuzi wa vyeti hivyo kutoka siku 14 za awali hadi siku tatu.

‘’Katika kipindi hiki, zaidi ya maombi 1,077 ya hati ya kutokuwa na pingamizi kwa wanaotaka kwenda kusoma elimu ya juu nje ya nchi yamewasilishwa TCU na kushughulikiwa na mfumo huu ni muhimu kwani unawapa fursa wananchi kufahamu uhalali wa programu wanazokwenda kusoma, hivyo kuwaepusha kupoteza rasilimali fedha za kusoma katika vyuo visivyotambulika,’’ amesema Prof. Kihampa.

Aidha, Prof. Kihampa alisema kupitia miongozo yake TCU imeweza kusajili wakala tatu zinazodahili wanafunzi wanaotaka kusoma elimu ya juu nje ya Tanzania, na kuzitaja wakala hizo ni pamoja na Global Education Link Ltd, DARWIN Education Agency Ltd na Yahoma Educational Ltd, pamoja na kupokea maombi ya wakala nyingine 7 zinazosubiri taratibu za usajili.

Prof. Kihampa alisema kwa mujibu muongozo huo, wakala wote hutakiwa kuwa na mikataba maalum baina yao na vyuo vilivyopo nje pamoja na Cheti maalum (NOC), na hivyo kuwataka wakala wote waliokidhi vigezo hivyo kutuma maombi yao TCU na kukamilisha usajili kwa wakati.