Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) imefungua dirisha la tatu la udahili kwa wanafunzi waliokosa nafasi na wangependa kujiunga na elimu ya juu kwa mwaka wa masomo wa 2020/2021.
Katibu Mtendaji wa TCU Prof. Charles Kihampa, amesema wamefikia uamuzi huo baada ya kupata maombi maalum kwa wadau waliotaka kuongezwa muda ili wenye sifa wapate fursa ya kujiunga na elimu ya juu.
Dirisha la awamu ya tatu limefunguliwa leo Oktoba 30 na litafungwa Novemba 4, mwaka huu ambapo TCU imetoa wito kwa waombaji kuhakikisha wanatumia vizuri fursa hiyo.
Aidha, katika hatua nyingine Profesa Kihampa ametoa wito kwa waombaji waliochaguliwa kwenye vyuo zaidi ya kimoja kuthibitisha udahili wao kwa vyuo wanavyovipenda kabla ya dirisha la tatu kufungwa.