TCRA yapiga ‘stop’ bei mpya za vifurushi

0
219

Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (TCRA), imesitisha kwa muda matumizi ya bei mpya ya vifurushi vya
data ili kutoa nafasi kwa watoa huduma kupanga upya bei za vifurushi kwa ufanisi na kufanya uchambuzi wa kina kwa ajili ya kulinda maslahi ya watumiaji.

Hatua hiyo imechukuliwa ikiwa na saa chache baada ya kampuni za mawasiliano ya simu kutoa maboresho ya vifurushi ambavyo vimeanza kutumika leo Aprili 2, 2021, ikiwa ni sehemu ya matakwa ya kanuni ndogo za vifurushi.

Baada ya vifurushi vipya kutolewa, baadhi ya wananchi kupitia mitandao ya kijamii wamelalamikia kile walichoeleza kuwa ni kupanda kwa gharama za vifurushi, tofauti na matarajio yao kuwa gharama zingepungua.

Mwanzoni mwa mwezi Februari mwaka huu, mamlaka hiyo iliandaa kanuni ndogo za vifurushi zenye lengo la kuweka utaratibu kwa watoa huduma namna ya kupanga vifurushi, bei na Muda wa matumizi ya vifurushi hivyo ambapo kanuni hizo zimeanza kutumika tarehe 2, aprili mwaka huu.

Baada ya kuanza kutumika kwa kanuni hizo, watumiaji wa mitandao hiyo wameonesha kutoelewa upangaji huo wa vifurushi na bei hali iliyozua sintofahamu.

Hivyo kwa sasa mamlaka imeelekeza huduma za vifurushi zirejee za awali huku ufumbuzi ukiendelea kutafutwa.