TCRA yakiweka kwenye uangalizi ‘Refresh’ ya Wasafi TV

0
182

Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekiweka chini ya uangalizi kipindi cha ‘Refresh’ kinachorishwa kwenye televisheni ya WASAFI kwa miezi mitatu kwa kosa la kutumia maudhui yasiyofaa kwenye jamii.

Akitoa hukumu hiyo leo mkoani Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Habbi Gunze amesema maudhui hayo yalirushwa na Wasafi Media kupitia mtandao wake wa ‘YouTube’ na runinga, ambayo yalihusu mahojiano kati ya msanii Zuhura Othman maarufu ‘Zuchu’ na mtangazaji Aaliyah Mohamed ambaye anakisimamia kipindi tajwa.

“Baada ya kutafakari kamati imeridhia pasipo na shaka kwamba Kampuni ya Wasafi kupitia kipindi chake cha ‘Refresh’ imekiuka kanuni za utangazaji wa redio na televisheni ya mwaka 2018 na kanuni za maudhui mtandaoni ya mwaka 2020,” amesema Gunze.

Pia imetoa onyo kali na kukiamuru kituo hicho kuomba radhi watazamaji wake na umma kwa ujumla kwa kipindi cha siku tatu kuanzia Januari 15 hadi 17 mwaka huu, huku pia mtangazaji wa kipindi hicho akiwekwa chini ya uangalizi kuanzia Leo hukumu iliposomwa.

Kamati imesema haki ya kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwenye Baraza la Ushindani wa Haki ya Biashara imewekwa wazi ndani ya siku 21 kuanzia siku ya kutolewa uamuzi huo.

Kutokana na kosa hilo kamati hiyo imeitaka WASAFI Media kuzingatia misingi ya sheria, kanuni na kusimamia weledi katika kuhariri na kutoa maudhui yenye tija kwa jamii ili kuepusha matatizo yanayoweza kujitokeza.