TCRA yaitoza Passion FM faini milioni 9

0
586

Kamati ya Maudhui ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) imekitaka kituo cha radio cha Passion FM kulipa faini ya shilingi milioni 9 ndani ya siku thelathini na kumuomba radhi Hadija Ally mkazi wa Chanika jijini Dar es Salaam mara tatu kwa siku tatu mfululizo kupitia kipindi cha Jogoo la Shamba.

Hayo yamejiri baada ya kituo hicho cha redio kukiuka kanuni za mawasiliano ya kielektroniki na posta kwa kwa kutangaza taarifa za shutuma dhidi ya mwanamama huyo bila ya uthibitisho kutoka kwake hali inayotafsiriwa kutofuata mizania ya kihabari.

Akitoa adhabu hiyo Mwenyekiti wa Kamati ya Maudhui ya TCRA, Valerie Msoka amesema kuwa adhabu hiyo imetolewa kwa mujibu wa sheria ikiwa ni baada ya kamati hiyo kusikiliza pande zote mbili .

Hata hivyo kamati hiyo imekipa onyo kituo hicho na kukishauri kutumia waandishi wa habari wenye taaluma ya habari na wahariri wenye weledi, wanaozingatia kanuni, sheria na maadili ya uandishi wa habari.