Kwa siku za hivi karibuni kumekuwepo na taarifa katika mitandao ya kijamii zikidai kuwa kinywaji cha ukwaju kinachotengenezwa na kampuni ya Bakhresa Food Products Co. Ltd kwamba si salama kutokana na kuwa na kemikali ijulikanayo kama Benzene.
Wakati madai hayo yakizidi kushika kasi, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limeingilia kati na kuwataka wananchi kupuuza madai hayo kwani kinywaji hicho ni salama kwani kimethibitishwa ubora wake kwa leseni Na. 1159 kwa kiwango cha kitaifa Na. TZS 585:2011.
TBS imeongeza kuwa vitunzio (preservatives) vya Sodium Benzoate na Ascobic Acid hutumika katika kuhifadhi vyakula na vinywaji mbalimbali kwa kiasi kinachokubalika na vinaruhusiwa kwa mujibu wa viwango na miongozo ya kitaifa na kimataifa.
Kemikali hizo kwa mujibu wa TBS hutumika kuhifadhi vyakula na vinywaji endapo mazingira ya uzalishaji na uhifadhi yatakapokuwa kama ifuatavyo:
i) Hali joto ikizidi nyuzi joto 50
ii) Hali ya tindikali (pH) inapokuwa chini ya 2
iii) Kifungashio kinachoruhusu mwanga
iv) Madini kama chuma na shaba yanayozidi kiwango kinachokubaliwa
v) Kiwango cha vitunzio kuzidi kupita kiasi
Aidha, TBS imewataka wananchi kuepuka kutoa taarifa ambazo zinazua taharuki na kupotosha jamii.