TBC yawashika mkono watoto wa Malaika Kids

0
139

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limetoa msaada wa vyakula vya aina mbalimbali kwa watoto wanaolelewa kwenye kituo cha Malaika Kids kilichopo Mwananyamala mkoani Dar es Salaam.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBC Dkt. Ayub Rioba Chacha wakati wa kukabidhi msaada huo, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TBC Catherine Nchimbi amesema, hatua hiyo ni Mwendelezo wa shirika hilo kujitoa kwa jamii.

Nchimbi amewaomba wadau wengine kuendelea kutoa misaada kwa wenye uhitaji ikiwa moja ya njia ya kuwafanya wawe na furaha.

Kwa upande wake mwanzilishi wa kituo hicho cha kulea watoto cha Malaika Kids Najma Manji ameishukru TBC kwa msaada huo na kutoa wito kwa jamii kuendelea kuwasaidia watoto wenye uhitaji katika jamii.

Wakizungumza na TBC, baadhi ya watoto wanaolelewa katika kituo hicho wamelishukuru Shirika la Utangazaji Tanzania kwa kuwapatia msaada huo na kusema bado wanakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja na kukosa ada za shule.

Msaada wa vyakula uliotolewa na TBC kwa kituo hicho cha kulea watoto cha Malaika Kids chenye jumla ya watoto 30 ni pamoja na mchele, unga, sukari na mafuta ya kupikia.