Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wamepanda miti 500 katika Shule ya Sekondari Bulale iliyopo katika Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza.
Akizungumza wakati wa zoezi la kupanda miti katika kampeni ya ‘Mti wa Mama na 27 ya Kijani’, Mkuu wa TBC Kanda ya Ziwa, Mhandisi Zablon Mafuru amesema kampeni hii inalenga kuifanya Tanzania kuwa ya kijani kwa kumuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni kinara katika kulinda na kuhifadhi mazingira. Kwa mujibu wa kampeni hiyo, kila tarehe 27 ya kila mwezi ni ya kupanda miti.
Kwa upande wake, Meneja wa TFS Kanda ya Ziwa, Mohamed Bakari, amesema zoezi la upandaji miti ni endelevu ili kufikia malengo ya serikali ya kuifanya Tanzania kuwa ya kijani kupitia upandaji wa miti.