TBC yamwaga fedha TFF, kurusha matangazo ya mpira wa miguu

0
210

Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limeingia mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wa urushaji wa matangazo ya mpira wa miguu kwa njia ya redio kwa kipindi cha miaka 10, wenye thamani ya shilingi bilioni 3.54.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Mratibu wa Miradi na Masoko, Gabriel Nderumaki amesema mkataba huo unaifanya TBC kuwa chombo pekee chenye haki ya kurusha matangazo ya mpira wa miguu wa njia ya redio.

“Huu mkataba unatufanya kuwa redio pekee yenye uhalali wa kurusha matangazo ya mpira wa miguu nchini, kwa hiyo yeyote anayehitaji kurusha lazima atuone,” amesema Nderumaki.

Kwa upande wake Rais wa TFF, Wallace Karia ameipongeza TBC kwa uthubutu wa kuweka fedha hiyo kwenye michezo kwani ndio mkataba wa kwanza mkubwa kuingiwa na chombo cha habari cha redio kwenye urushaji wa matangazo ya mpira wa miguu.

“Nimeingia kwenye rekodi nyingine ya kuwa Rais wa shirikisho aliyeingia mkataba mnono na redio katika kurusha ligi kuu, hili najipongeza,” amesema Karia.

Fedha hizo pia zitavinufaisha vilabu vinavyoshiriki Ligi Kuu ya Tanzania.