Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limesaini Mkataba wa Makubaliano (M.O.U) na Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) kwa ajili ya ujenzi wa vituo vipya vitano vya redio vya shirika hilo katika maeneo ya mipakani ikiwemo Kyela, Ngara, Ludewa, Mlimba na Ruangwa.
Hafla ya utiliaji saini wa mkataba huo wenye thamani ya shilingi bilioni 1 imefanyika katika ofisi za UCSAF jijini Dodoma na kuhudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBC, Dkt. Ayub Rioba pamoja na viongozi na wageni mbalimbali.
Ujenzi wa vituo vipya utawezesha kuongeza na kuimarisha usikivu wa TBC katika maeneo mbalimbali nchini ikiwa ni mkakati wa serikali kuhakikisha kuwa chombo hiki cha umma kinawafikia watu wengi zaidi.
Hivi karibuni akizungumzia mkakati wa kuboresha usikivu wa TBC, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa, na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alieleza mikakati itakayotumika kuimarisha usikivu wa TBC ambayo ni pamoja na kubadilisha mitambo ya zamani na kuweka mipya na kuhamisha mitambo kutoka sehemu ambayo mawimbi ya FM hayafiki na kuipeleka maeneo ya vilima vilivyopo juu zaidi.