Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt Harrison Mwakyembe amesema kuwa kupitia uwekezaji unaofanyika katika bajeti ya maendeleo, Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) limeendelea kupanua usikivu kutoka asilimia 54 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 63 mwaka huu wa 2019.
Akiwakilisha Bungeni jijini Dodoma, bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 Waziri Mwakyembe amesema kuwa, lengo la TBC ni kuhakikisha usikivu wa redio kwa wilaya 117 nchini, unafikia asilimia 73 mwaka ujao wa fedha.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mjumbe wa kamati hiyo Deogratius Ngalawa amesifu maboresho yanayoendelea kufanywa ndani ya Shirika la Utangazaji Tanzania.
Baadhi ya wabunge waliochangia bajeti hiyo ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kwa mwaka wa fedha wa 2019/2020, wameiomba serikali kupitia wizara hiyo kuhimiza matumizi Kiswahili fasaha hasa kwa wasanii.