Mkurugenzi wa Huduma za Redio wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) Aisha Dachi kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Dkt. Ayub Rioba Chacha, amekabidhi rasmi kwa Mkandarasi eneo la kujengwa uzio lililopo katika ofisi za TBC barabara ya Nyerere.
Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika kwenye eneo la ujenzi, Dachi amesema zoezi hilo linatakiwa kuanza mara moja baada ya makabidhiano .
Ameongeza kuwa lengo la ujenzi wa uzio huo ni kulinda na kuhifadhi mitambo ya kurusha matangazo ya redio ambayo ipo hatarini kudhurika kutokana kuendeshwa kwa shughuli za kibiashara katika na eneo hilo.
Awali baadhi ya mitambo ilinusurika kuungua moto uliotokana na shughuli za kibiashara zilizokuwa zikiendelea katika eneo hilo huku uharibifu wa mazingira ukifanyika ikiwemo kukata miti bila utaratibu.
Kwa upande wake Mkandarasi wa ujenzi wa mradi huo wa uzio, Mhandisi Boniphace Marwa kutoka Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (SUMAJKT) amesema, shirika hilo lipo tayari kutekeleza ujenzi huo kulingana na makubaliano.
Baadhi ya wajasiriamali waolivamia eneo la ofisi hizo za TBC barabara ya Nyerere wamekiri kutambua kuwa wamevamia eneo hilo na kwamba ni hatari kwa mitambo ya TBC na kusema kuwa wapo tayari kuondoka.
Ujenzi wa uzio huo unatarajia kukamilika ndani ya kipindi cha siku 90 kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa baina ya TBC na SUMA JKT.