Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Damas Ndumbaro ametoa muda wa takribani wiki tatu kuanzia leo kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kuzipitia upya kanuni zinazowezesha watu binafsi kuanzisha na kumiliki mashamba ya wanyamapori.
Dkt. Ndumbaro ametoa muda huo mjini Moshi mkoani Kilimanjaro wakati akizungumza na wamiliki wenye mashamba yenye wanyamapori kanda ya Kaskazini, kwa lengo la kujadili changamoto za uendeshaji na umiliki wa mashamba hayo.
Amesema wametambua urasimu uliopo kwenye utoaji wa leseni kwa watu binafsi wanaotaka kuanzisha na kumiliki mashamba ya Wanyamapori, hivyo kurekebishwa kwa kanuni hizo kutasaidia kuondoa vikwazo kwa watu hao.
Dkt. Ndumbaro pia ameitaka TAWA kuendelea kuyafanyia kazi maombi ya leseni za watu binafsi wanaotaka kuanzisha na kumiliki mashamba yenye Wanyamapori yaliyopokelewa haraka iwezekanavyo, kwani bila kufanya hivyo Wawezekaji watapotea.
Kwa upande wao baadhi ya wamiliki wa mashamba yenye Wanyamapori wamesema kauli ya Waziri wa Maliasili na Utalii imewapa muelekeo mpya kwa kuwa kanuni zilizopo kwa sasa haziwasaidii katika kufuga wanyamapori kwenye mashamba yao.