TAWA kuongeza ulinzi wa rasilimali

0
139

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mabula Nyanda amesema, mwelekeo wa
wizara ya Maliasili na Utalii ni kuhakikisha rasilimali za nchi zinalindwa ikiwa ni pamoja na kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo katika maeneo yote yanayosimamiwa kisheria.

Kamishna Mabula
ameyasema hayo wakati wa mkutano wake na Wahifadhi wa Pori la Akiba Muhesi lililopo wilayani Manyoni mkoani Singida katika siku ya pili ya ziara yake Kanda ya Kati.

“kubwa lililotuleta hapa, ni kutoa mwelekeo wa wizara ya Maliasili na Utalii kufuatia mabadiliko ya uongozi wa juu” amesema Kamishna Mabula na kuongeza kuwa

“Kwa sasa mwelekeo wa uongozi wa juu wa wizara, kwanza kabisa wanataka tuhakikishe maeneo na rasilimali zilizopo katika maeneo tunayoyasimamia zinakuwa salama, tuzilinde kwa nguvu zote”.

Kamishna Mabula amesema ili kufanikisha kazi ya ulinzi wa rasilimali za nchi, wahifadhi wote wa TAWA hasa wa Pori la Akiba Muhesi wanapaswa kuzifahamu vema rasilimali walizonazo, kujua mahali zilipo na kuzitambua.

Amewaelekeza Wahifadhi wote wa Pori hilo kwa kutumia GPS na teknolojia nyingine kuhakikisha wanazitambua rasilimali zilizopo katika maeneo yao.