Tanzania yatoa msaada kwa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe

0
505

Tanzania imetoa msaada wa dawa, chakula na vifaa vya kujihifadhi kwa nchi za Msumbiji, Malawi na Zimbabwe kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa kimbunga cha Idai kilichosababisha mafuriko yaliyozikumba nchi hizo.

Msaada huo umekabidhiwa kwa mabalozi wa nchi hizo wanaoziwakilisha nchi zao hapa nchini na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.

Sehemu ya msaada huo unaokwenda katika nchi za Zimbabwe na Msumbiji umesafirishwa hii leo kwa kutumia ndege za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Akizungumza wakati zoezi la kupakia msaada huo katika ndege ya Jeshi likiendelea,  Profesa Kabudi amesema kuwa Rais John Magufuli ameagiza kutolewa kwa msaada huo pamoja na salamu za pole kwa Marais wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe na wananchi wa nchi hizo kwa madhara makubwa waliyoyapata kutokana na mafuriko hayo.

Kwa hivyo Rais Magufuli baada ya kupata taarifa hizi na kuzungumza na Marais wenzake wa Msumbiji, Malawi na Zimbabwe, Tanzania imeona ni vyema kutokana na undugu wetu, umoja wetu na ujirani wetu tuweze kuwapelekea msaada angalau kidogo wa dawa na chakula na pia kuwapa pole kwa maafa haya makubwa yaliyowapata” amesema Profesa  Kabudi.

Amebainisha kuwa  kati ya msaada huo, malori Saba yenye shehena ya Tani 200 za mahindi yanaondoka leo kutoka Mbeya kwenda nchini Malawi ambako taarifa zinaonesha watu 122 wamefariki dunia na wengine zaidi ya Elfu Moja hawana mahali pa kuishi, tani Saba za mchele, dawa na vifaa vya kujihifadhi zinaondoka Dar es Salaam kwa kutumia ndege ya Jeshi kwenda Msumbiji ambako watu 221 wamefariki dunia na tani nyingine Saba za mchele, chakula na vifaa vya kujifadhi zinaondoka Dar es Salaam kwa ndege ya Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania kwenda nchini Zimbabwe ambako watu 98 wamefariki dunia kutokana na mafuriko hayo yaliyosababishwa na kimbunga Idai.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amesema kuwa serikali imetoa tani 24 za dawa ambapo kila nchi itapatiwa tani Nane zinazojumuisha dawa za kuzuia maambukizi ya magonjwa, dawa za magonjwa ya tumbo, dawa za kutuliza maumivu, dripu, shuka, blanketi, magodoro na vyandarua.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya nchi yake, Balozi wa Msumbiji nchini Monica Mussa amemshukuru Rais Magufuli na serikali ya Tanzania kwa msaada huo ambao amesema kuwa utasaidia kunusuru maisha ya watu wengi ambao hawana chakula, wanahitaji dawa na wanahitaji malazi.

Nae Balozi wa Malawi hapa nchini Glad Chembe Munthali amemshukuru Rais Magufuli na kueleza kuwa msaada huo wa haraka umedhihirisha udugu, ujirani na umoja wa dhati uliopo kati ya Tanzania na Malawi.

Kaimu Balozi wa Zimbabwe hapa nchini Martin Chavenika pamoja na kutoa shukrani zake za dhati,  amemhakikishia Rais Magufuli na Serikali kwa ujumla kuwa msaada huo utawafikia walengwa.

Mkuu wa Mafunzo na Utendaji Kivita wa Kamandi ya Jeshi la Anga Brigedia  Jenerali Francis Shirima amesema kuwa JWTZ itahakikisha msaada wote uliotolewa unafika hii leo kwa nchi hizo na kukabidhiwa kwa wahusika.