Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema mataifa yanapaswa kujitoa upya na kuazimia kuongeza uwekezaji katika sekta ya elimu, ili kuhakikisha watoto wanapata elimu iliyo bora na ya uhakika.
Makamu wa Rais amesema hayo jijini New York, Marekani alipokuwa akihutubia mkutano wa Umoja wa Mataifa uliobeba ajenda ya mageuzi katika sekta ya elimu ulioshirikisha wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa mbalimbali, wakuu wa taasisi na mashirika pamoja na wadau wa sekta ya elimu.
Amesema kwa kuwa elimu ni sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo 2030, hakuna budi kuchukua hatua katika kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo.
Dkt. Mpango amesema, kupatikana kwa elimu bora kutapunguza matabaka katika ajira pamoja na kipato baina ya wananchi.
Amesema tayari serikali ya Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na kuanza mchakato wa kuboresha mitaala kwa kuwashirikisha wadau wa elimu, kuwekeza katika vyuo vya ufundi stadi na mafunzo , kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari pamoja na kuongeza bajeti ya wizara husika kufikia asilimia 18 ya bajeti yote ya serikali.
Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yupo nchini Marekani kumwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA).