Tanzania yasisitiza diplomasia kumaliza mgogoro wa Russia na Ukraine

0
342

 
Serikali ya Tanzania imetoa ufafanuzi kuhusu sababu ya kupiga kura ya kutofungamana na upande wowote katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu mgogoro unaoendelea kati ya Russia na Ukraine, huku ikisisitiza pande zote mbili kutafuta suluhu katika meza ya mazungumzo.
 
Waziri wa mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Balozi Liberata Mulamula amesema  Sera ya Tanzania kuhusu namna ya kutatua migogoro inapojitokeza ni kwa kutumia njia za kidiplomasia.
 
 
Amesisitiza kuwa sera ya Mambo ya Nje ya Tanzania haijabadilika tangu Uhuru,  na kwamba inaamini hakuna mgogoro ambao hauwezi kutatulika  hasa panapokuwepo na utashi na nia njema ya kumaliza mgogoro huo.
 
Balozi Mulamula amesema njia ya kidiplomasia ndio chaguo sahihi kwa Tanzania kuhusu namna bora ya kumaliza mgogoro kati ya Russia  na Ukraine.
 
Kuhusu endapo Tanzania imeathirika na vita inayoendelea kati ya Russia  na Ukraine, Balozi Mulamula amesema madhara yanayotokana na vita hiyo yanajionesha dhahiri, likiwemo lile la baadhi ya Wanafunzi wa Kitanzania waliokuwa wanasoma nchini Ukraine kukatisha masomo yao na kurejea nchini wakisubiria vita kumalizika.
 
Kutokana na vita inayoendelea kati ya Russia na Ukraine, Tanzania ililazimika kuwaondoa raia wake nchini Ukraine, kati yao ni takribani Wanafunzi 300 waliokuwa wakisomea udaktari nchini humo