Katika jitihada za kutekeleza diplomasia ya uchumi kwa vitendo, Tanzania kwa mara ya kwanza inashiriki katika maonesho ya kimataifa ya kilimo yanayojulikana kama MACFRUT FIERA yanayoendelea mjini Rimini nchini Italia.
Maonesho hayo yanayofanyika kila mwaka yanawakutanisha wazalishaji, wanunuzi na wauzaji wa bidhaa za kilimo cha mboga na matunda, ufugaji wa kuku na mashine za kisasa zinazotumika katika kilimo.
Ubalozi wa Tanzania nchini Italia kwa kushirikiana na wizara ya Kilimo unashiriki maonesho hayo huku tunda la mwaka huu likiwa ni parachichi.
Akizungumza wakati wa maonesho hayo, balozi wa Tanzania nchini Italia, Mahmoud Thabit Kombo amewasihi wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Italia kuwekeza Tanzania.
“Nawahakikishia kuwa Tanzania imeboresha mazingira ya uwekezaji kwa kupunguza kero zilizokuwa hapo awali na kwamba Watanzania wapo tayari kuwapokea.” amesema Balozi Kombo