Tanzania yashinda tuzo maonesho ya utalii Korea Kusini

0
199

Tanzania imetunukiwa tuzo kwa kuwa na banda bora lenye ubunifu wa kutangaza utalii katika maonesho ya 37 ya utalii ya Seoul International Travel Fair (SITF) jijini Seoul nchini Korea Kusini kuanzia tarehe 23 – 26 Juni 2022.

“Tuzo hii ni ishara nzuri ya ushirikiano kati ya Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini, Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na wadau wa Utalii wa Tanzania katika kuandaa ushiriki wa Tanzania katika maonesho  ya SITF.  Tutaendelea kuzijongea fursa za kutangaza utalii wa Tanzania na kushiriki katika matukio mbalimbali yatayofanyika hapa Korea,” amesema Balozi wa Tanzania nchini Togolani Mavura.

Banda la Tanzania lilipambwa kwa kuonesha vivutio mbalimbali vinavyopatikana nchini Tanzania ambapo picha za utalii wa kutamaduni, Mlima Kilimanjaro, fukwe za Zanzibar, nyumbu wanaovuka Mto Mara, na madini ya Tanzanite zimewavutia wageni wengi waliotembelea maonesho hayo.

Katika Banda la Tanzania wananchi wa Korea waliweza kujitokeza kwa wingi kunywa na  kufurahia ladha ya kahawa ya Tanzania, tukio hili lilichangia Banda la Tanzania kutembelewa na wageni wengi. Kahawa iliyotumika kwenye maonesho haya ni ile inayolimwa katika wilaya ya mbinga mkoani Ruvuma.

Aidha, Wanawake wengi wa waliotembelea banda la Tanzania walivutiwa sana na ususi wa nywele  ambapo walijitokeza kwa wingi kusuka nywele zao, jambo ambalo walionyesha kulifurahia sana.

Kwa upande wa Bodi ya Utalii Tanzania, Afisa Habari na Uhusiano, Augustina Makoye amesema “Tunaendelea kubuni njia mbalimbali za kutangaza utalii wa Tanzania ili vivutio vya Tanzania viweze kujulikana zaidi katika soko hili ambalo wananchi wengi wameonesha kuvutiwa zaidi na vitu vya kiutamaduni, tutaendelea kuliwekea mkakati wa kutangaza utalii wa kiutamaduni kwa vitendo ili tuweze kuwavitia watalii wengi wa nchi ya Korea Kusini.