Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mashimba Ndaki amesema kwa sasa Tanzania imejenga uwezo katika uzalishaji wa chanjo za mifugo na hivyo kusaidia kupambana na magonjwa mengi ya mifugo hapa nchini.
Waziri Ndaki amesema, uwepo wa viwanda vya kuzalisha chanjo hapa nchini kumesaidia uwepo wa ongezeko la chanjo hizo kutoka milioni 26 mpaka chanjo milioni 60 kwa hivi sasa.
Ameongeza kuwa hivi sasa Tanzania imejenga uwezo na kuongeza uzalishaji wa chanjo ambapo jumla ya chanjo 7, zinazalishwa hapa nchini na hivyo kusaidia kutibu mifugo ambayo awali ilikuwa inakufa kwa kukosa chanjo kwa wakati.
Kuhusu udhibiti wa magonjwa ya mifugo, Waziri Ndaki amesema, wameongeza kasi ya ujenzi wa majosho kutoka majosho 2438 mwaka 2020 hadi kufikia Majosho 2526 mwaka 2021.
Ndaki ameongeza kuwa katika bajeti ya mwaka huu wizara yake imepanga kujenga majosho mapya 170, katika Halmashauri ambazo zina mifugo mingi zaidi hapa nchini.
Ameongeza kuwa lengo la mkutano wa mwaka huu wa wadau wa mifugo ni kujadili na kuona namna sekta hiyo itakavyoweza kuchangia katika pato la Taifa.