Tanzania yaonesha tena mfano duniani

0
757

Tanzania imekuwa kati ya nchi za kwanza kufungua anga kwa kuruhusu safari za ndege kutoka nchi mbalimbali duniani kutua nchini baada ya usafiri wa anga kusitishwa kufuatia janga la ugonjwa wa Covid-19 lililoikumba dunia mwezi Desemba mwaka 2019.

Jitihada hizo za Serikali za kurejesha safari za ndege baada ya athari ya ugonjwa wa Covid-19 zimekuwa na manufaa ambapo Agosti 5, 2020 ndege ya Shirika la Ndege la Uholanzi (KLM) aina ya Boeing 777-200 ilitua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) ikiwa imebeba watalii.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mgwira amesema Serikali ilifuatilia kwa karibu hatua zote za kutua kwa ndege ya KLM ikiwa ni pamoja na kuikaribisha ndege hiyo kwa maji kama ilivyo utaratibu. Aidha, kufika kwa abiria hao nchini kumesababishwa na imani ambayo Serikali imeijengea dunia.

“Tumeijengea dunia imani kwamba nchi yetu ni salama na ugonjwa wa Covid-19 uliopokuja tulipata na hofu na sasa tuimeishinda hofu na tumewasaidia na wao kuishinda hofu hiyo kwa kutojifungia ndani,” amesema Mghwira.

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa KIA, Christine Mwakatobe amesema kuwa kutua kwa ndege ya KLM nchini kunadhihirisha namna ambavyo Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga (IATA) wameiona Tanzania ni sehemu salama.

Aidha, Mwkatobe alisema hatua hiyo ni muendelezo wa kuirejesha sekta ya utalii nchini ambayo iliathirika kwa kiasi kikubwa kufuatia janga la ugonjwa wa Covid-19.

Hivi karibuni mashirika kadhaa ya ndege yakiwemo Qatar, Crystal, na Rwanda Air yamefanya safari zake nchini baada ya kuridhishwa na usalama wa abiria na pamoja na mali, huku hali ya maambukizi ya ugonjwa wa Covid-19 ikiwa shwari.