Tanzania yang’ara mkutano wa CITES

0
102

Tanzania imechaguliwa kuwa mjumbe wa akiba wa Kamati Kuu upande wa Kamati ya Wanyamapori na mjumbe wa Kamati ya Mimea kwa kipindi cha miaka mitatu kwa nchi wanachama wa mkataba wa Kimataifa wa Biashara ya Wanyamapori na Mimea iliyo hatarini kutoweka (CITES).

Hayo yamejiri wakati wa mkutano wa 19 wa nchi wanachama wa CITES uliofanyika nchini Panama.

Akizungumza mara ya uchaguzi huo Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Pindi Chana akiwa ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo wa CITES amesema, hatua hiyo inaipa nafasi nzuri Tanzania ya kusimamia na kutetea masuala ya kimkakati yenye maslahi mapana kwa uhifadhi na biashara ya kimataifa ya mazao ya wanyamapori, misitu na uvuvi.

Mkutano huo umejadili ajenda 89 yakiwemo mapendekezo 52 ya kuweka, kuondoa au kubadili hadhi ya wanyamapori na mimea katika makundi ya mkataba wa CITES, ambapo Tanzania imeshiriki kujadili mapendekezo 16 ya kuweka wanyamapori na mimea katika makundi ya mkataba huo.

Mkutano huo umehudhuriwa na wajumbe takribani elfu tatu kutoka nchi 153 ambazo ni wanachama wa CITES.