Tanzania yalia na mzigo wa Wakimbizi

0
191

Tanzania imeuomba Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kimataifa kuongeza jitihada katika kutafuta amani kwenye maeneo yenye migogoro Barani afrika ili kuipunguzia mzigo wa Wakimbizi ilioubeba kwa muda mrefu.

Ombi hilo limetolewa na Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan katika siku ya kwanza ya mkutano wa 33 wa kawaida wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika unaofanyika mjini Addis Ababa nchini Ethiopia.

Amesema kuwa endapo Umoja wa Afrika na Jumuiya ya Kimataifa wataongeza nguvu katika kutafuta suluhu kwenye maeneo yenye migogoro, Viongozi wa maeneo husika pia wataelekeza nguvu kubwa  katika kuwaletea Wananchi maendeleo na hivyo kupunguza umasikini katika Bara la Afrika linaloonekana kama limekithiri kwa migogoro na mapigano.
 
Mkutano huo wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika umeshuhudia tukio la kubadilishana uongozi ambapo Mwenyekiti anayemaliza muda wake Rais Abdel Fattah Al-Sisi wa Misri amekabidhi Uenyekiti kwa Rais Cyrill Ramaphosa wa Afrika Kusini.