Tanzania yakamilisha mkakati wa kurejesha mandhari ya misitu

0
212
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja akijibu maswali ya wabunge katika kikao cha nne cha mkutano wa tisa wa Bunge la 12.

Tanzania imekamilisha maandalizi ya mkakati wa kitaifa wa kurejesha mandhari ya misitu wenye lengo la kuongoa ardhi iliyoharibika kutokana na shughuli za kibinadamu.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Donge, Mohamed Soud aliyetaka kujua Kampeni ya AFR imetekelezwa kwa kiasi gani.

Amesema mkakati huo unatarajiwa kuwasilishwa katika Mkutano wa 27 wa nchi wanachama wa kujadili masuala ya mazingira ulioanza Oktoba 30,2022 nchini Misri.

Sambamba na hilo amesema Serikali imesaini makubaliano ya kurejesha mandhari ya Kiafrika- kupitia kampeni ya AFR 100 iliyokuwa na azma ya kuongoa hekta milioni 100 za ardhi iliyoharibiwa barani Afrika.

Kupitia kampeni hiyo Tanzania iliahidi kuongoa hekta milioni 5.2 za ardhi iliyoharibiwa ambapo kwa sasa inatekelezwa kwa kuondoa wavamizi na kurejesha ardhi iliyoathiriwa, kuimarisha usimamizi wa misitu ya mikoko, kutoa elimu ya kudhibiti moto wa msituni ili kulinda uoto wa asili na kutekeleza Mpango wa Dodoma ya Kijani.