Tanzania yafanya mazungumzo na Ethiopia kuhusu Wahamiaji

0
206
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akisalimiana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia, Dkt. Workneh Gebeyehu walipokutana kwa ajili ya mazungumzo mjini Addis Ababa, Ethiopia, kando ya Mkutano wa 33 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika.

Tanzania imeishauri Ethiopia kuchunguza kiini cha raia wake kuondoka nchini humo kinyume na utaratibu, jambo linalosababisha  mrundikano wa wafungwa ambao wanakamatwa katika nchi wanazopita kama wahamiaji ikiwemo Tanzania.

Ushauri huo umetolewa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Profesa Palamagamba Kabudi mjini Addis Ababa  nchini Ethiopia,  kando ya mkutano wa 33 wa wakuu wa nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika mara baada ya kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ethiopia Dkt Workneh Gebeyehu.

Amemueleza Dkt Gebeyehu kuwa mpaka sasa zaidi ya raia 1,300 wa Ethiopia wanashikiliwa katika magereza mbalimbali nchini Tanzania huku idadi ya wanaoendelea kukamatwa ikiongezeka.

Wakati wa mazungumzo hayo ya Profesa Kabudi na Dkt Gebeyehu,  Tanzania na Ethiopia zimekubaliana kuchukua hatua za pamoja zitakazowezesha kurejeshwa wafungwa na wahamiaji wa  Ethiopia wanaoshikiliwa Tanzania kwa utaratibu utakaokubalika.

Waziri huyo wa Mambo ya Nje wa Ethiopia amekiri kuwepo kwa tatizo la vijana wa nchi hiyo kuondoka kinyume cha utaratibu na kuitumia Tanzania kama mapito wakielekea katika nchi za Kusini mwa Afrika na Ulaya, hivyo wataendelea kuweka mikakati madhubuti ili  kukabiliana na hali hiyo.

Pia ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano wake katika suala la Wahamiaji kwa kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu aaia wa Ethiopia wanaoshikiliwa Tanzania.