Tanzania yafanya kongamano la uwekezaji katika sekta ya Utalii Dubai

0
187

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii Mary Masanja amesema, uwekezaji katika sekta ya utalii utasaidia kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini Tanzania pamoja na kujenga mahusiano ya uwekezaji kwenye Sekta ya Utalii.

Naibu waziri Masanja amesema kuna umuhimu mkubwa kutumia fursa ya maonesho ya Expo 2020 Dubai kutangaza na kuelezea fursa za uwekezaji zilizopo nchini.

Ameongeza kuwa, nchini Tanzania kuna fursa nyingi za uwekezaji katika maeneo ya mijini na sehemu mahsusi za utalii zikiwemo za kiutamaduni na kihistoria, Maeneo ya hoteli za kitalii, migahawa, maeneo ya michezo na utalii ikolojia.

Kongamano hilo limehudhiriwa na Mkurugenzi wa Idara ya Uchumi ya Diplomasia Dubai, Balozi Edwin Rutageruka, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Allan Kijazi, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Utalii nchini TTB, Betrita Lyimo, Hafsa Mbanga kutoka Kamisheni ya Utalii Zanzibar pamoja na Jumuiya ya Wafanyabiashara Dubai ikiwa ni sehemu ya Makongamano yaliyoandaliwa na Tanzania kwenye maonesho ya Expo 2020 Dubai.