Tanzania na Vatican zimeahidi kuendelea kuhimiza amani na utulivu katika masuala yenye changamoto mbalimbali, ili kuwezesha uwepo wa amani duniani.
Pande hizo pia zimeahidi kuendelea kutambua mchango unaotolewa na Kiongozi wa Kanisa Katoliki dunisni Baba Mtakatifu Francis katika kuhimiza amani, utulivu na usalama duniani.
Ahadi hiyo imetolewa mkoani Dar es salaam na Waziri Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Profesa Palamagamba Kabudi alipokutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Vatican nchini Askofu Mkuu Marek Solczynski.
Profesa kabudi amesema Tanzania na Vatican kwa kutambua umuhimu wa amani, zimeahidi kuendelea kushirikiana katika mikutano ya Umoja wa Mataifa kuhimiza amani, utulivu na mshikamano katika masuala mbalimbali yenye changamoto duniani.
Amesema kwa sasa dunia inakabiliwa na changamoto nyingi ambazo zinahitaji mshikamano wa mataifa yote duniani ili kuweza kuyakabili, hii ikiwa ni pamoja na masuala yanayohusu amani, utulivu, majanga na magonjwa ya mlipuko kama vile corona.
Kwa upande wake Balozi wa Vatican nchini Askofu Mkuu Solczynski amesema kuwa, Vatican itaendelea kuimarisha mahusiano yake ya kidiplomasia na Tanzania kwa masuala yenye maslahi ya haki, utu, amani na utulivu.