Tanzania na Uganda zanufaika na ushirikiano

0
2669

Tanzania na Uganda zimepata mafanikio makubwa kupitia mikutano ya Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) iliyofanyika jijini Arusha mwezi Aprili mwaka huu na ule uliofanyika mjini Kampala nchini Uganda na kumalizika Agosti 23 mwaka huu.

Kauli hiyo imetolewa na waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania na Ushirikiano wa Afrika Mashariki wa Tanzania Balozi Augustine Mahiga na mwenzake wa Uganda, -Sam Kutesa wakati wa ufunguzi wa mkutano uliofanyika mjini Kampala.

Wametaja mafanikio yaliyopatikana kuwa ni pamoja na kusainiwa kwa Mikataba ya Makubaliano tisa ikiwemo Mikataba ya kushirikiana katika uendelezaji wa bomba la kusafirisha gesi asilia kutoka Dar es salaam hadi Uganda na ile ya ushirikiano katika masuala ya elimu na mafunzo.

Mikataba hiyo inalenga kurahisisha ukuaji wa uchumi wa nchi hizo mbili ili kutimiza azma ya viongozi wa nchi hizo John Magufuli na Yoweri Museveni wa Uganda ya kukuza biashara kati ya nchi hizo.

Kufuatia mikataba hiyo miradi mbalimbali ipo katika hatua tofauti za utekelezaji ikiwemo mradi wa kuzalisha umeme wa Kikagati – Murongo uliopangwa kukamilika mwaka 2020.

Pia Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) litaanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es salaam hadi Entebbe mwishoni mwa mwezi Agosti mwaka huu kufuatia kusainiwa kwa mkataba wa masuala ya anga katika mkutano uliofanyika jijini Arusha.