Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) zimetiliana saini mikataba mitatu ya mikopo yenye masharti nafuu yenye jumla ya shilingi bilioni 592 kwa ajili ya miradi ya usambazaji wa umeme vijijini, mradi wa umeme wa kuunganisha Tanzania na Zambia pamoja na kukamilisha mradi wa maji safi na maji taka katika miji inayozunguka Ziwa Victoria.
Wakati wa kusaini mikataba hiyo Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James amesema kuwa mradi wa usambazaji wa umeme vijijini utagharimu Euro milioni 100 (shilingi bilioni 257.64) na utasambazwa katika mikoa 16 ya Tanzania Bara na mradi wa umeme wa kuunganisha Tanzania na Zambia.
James amesema miradi yote mitatu ambayo imesainiwa inawiana na Dira ya Maendeleo ya Tanzania ya mwaka 2025, ambayo inaongoza juhudi za kuleta maendeleo nchini hadi mwaka 2025 na kwa sasa inatekelezwa kupitia Awamu ya Pili ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP II) 2016/17 – 2020/21.
Ameongeza kuwa malengo ya dira ni kuinua, kuratibu na kuelekeza juhudi za Watanzania, fikra na rasilimali za Taifa kwenye sekta muhimu ambazo zitawezesha nchi kufikia maendeleo na kuhimili ushindani mkubwa wa kiuchumi.
Kwa upande wa mradi wa maji, James amesema kukamilika kwa mradi huo kutawezesha upatikanaji wa maji kutoka mita za ujazo 33,000 hadi kufikia mita za ujazo 108,000 kwa siku pamoja na kuwezesha Mji wa Morogoro kupata kiwango cha mahitaji ya maji safi kinachokadiriwa kuwa mita za ujazo 126,253 kwa siku, ifikapo mwaka 2035.
Tanzania imekuwa ikinufaika na ufadhili wa AFD hususan katika sekta za nishati, maji, usafirishaji na kilimo kupitia idadi ya miradi mbalimbali inayoendelea na ile inayotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Miradi saba inayoendelea kutekelezwa katika sekta mbalimbali hapa nchini kupitia misaada na mikopo inayotolewa wa shirika hilo inafikia takriban Euro milioni 154.5 (shilingi bilioni 387.6).
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD), Stephanie Essombe ameahidi kuwa shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania ili kuhakikisha inafikia malengo yake katika kuboresha maisha ya wananchi hasa katika upatikanaji wa maji.
“Ushirikiano wa Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) ulioanza miaka 20 iliyopita umezidi kuimarika ambapo katika kipindi cha miaka 10 iliyopita shirika limewekeza kiasi cha Euro milioni 258 (takriban shilingi bilioni 655),” amesema Bi. Essombe.