Tanzania na Sweden kuimarisha ushirikiano

0
137

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amesema Sweden imepiga hatua katika sekta ya afya hasa kwa madaktari bingwa wa magonjwa ya moyo, hivyo kuna umuhimu kwa Taifa hilo kushirikiana na Tabzania katika kutoa mafunzo kwa madaktari.

Dkt. Mpango ameyasema hayo alipokutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Ann Linde mjini Stockholm.

Ameongeza kuwa Tanzania na Sweden zinaweza kurejesha ushirikiano uliokuwepo hapo awali katika sekta ya elimu ya juu uliochochea upatikanaji wa wataalamu mbalimbali nchini.

Amesema Tanzania na Sweden zimekua na ushirikiano mzuri wa muda mrefu na serikali ya awamu ya sita imelenga kuimarisha ushirikiano huo.

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Sweden, Ann Linde ameipongeza Tanzania kwa hatua mbalimbali inazoendelea kuchukua ikiwemo kuimarika kwa haki za binadamu, uhuru wa vyombo vya habari pamoja na demokrasia.

Amesema Tanzania imefanya jambo la muhimu kutoa haki kwa wanafunzi wa kike wanaopata ujauzito kuendelea na masomo kwa kutambua elimu ndio nguzo muhimu kwa maisha yao.

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango yupo nchini Sweden kuhudhuria mkutano wa Umoja wa Mataifa wa Stockholm +50 wenye lengo la kuchochea utekelezaji wa Malengo Endelevu ya Umoja wa Mataifa (Ajenda 2030) hususani katika upande wa mazingira na kujadili namna ya kurejesha uchumi endelevu katika kukabiliana na janga la UVIKO – 19.