Serikali za Tanzania na Rwanda zimekubaliana kuweka mazingira bora yatakayosaidia kuongeza ufanisi wa matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam, ikiwa ni moja ya njia za kusaidia kukuza uchumi wa nchi hizo mbili.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki January Makamba alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Kigali, Rwanda akiwa na Waziri mwenza wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Dkt. Vincent Biruta.
Rwanda imeongeza wigo wa matumizi ya Bandari ya Dar es Salaam kwa zaidi ya asilimia 80 kwa usafirishaji wa mizigo yake.
Mbali na usafirishaji, Waziri Makamba na Waziri Biruta wamejadili masuala mengine ya kipaumbele kwa nchi hizo mbili kushirikiana ikiwemo Nishati, Kilimo na Teknolojia.