Tanzania na China kuendelea kushirikiana

0
219

Na,Emmanuel Samwel TBC

Rais Samia Suluhu Hassan, ameitaka Wizara ya Mambo ya Nje na Wizara ya Ulinzi kuendeleza uhusiano mzuri baina ya watu wa China na Serikali ya Tanzania kwa ustawi wa Taifa.

Rais Samia ametoa wito huo wakati wa hafla ya kuzindua jengo jipya la Chuo Cha Taifa Cha Ulinzi Tanzania kilichopo Kunduchi mkoani Dar es Salaam ambalo limejengwa kwa msaada wa Jeshi la Ukombozi la watu wa China.

Katika hotuba yake Rais Samia amebainisha kuwa watu wa China ni wadau wa Serikali ya Tanzania katika nyanja zote za maendeleo hivyo kusisitiza uhusiano huo ulioasisiwa na viongozi wa kitaifa kwa miaka 57 iliyopita hivyo ni vyema kuendelezwa.

“Matunda yanayoshuhudiwa leo ni jukwaa imara ulioasisiwa kwa miaka 57 iliyopita na Mwalimu Nyerere na aliyekuwa muasisi wa Taifa la China Mao Sentung ni wa kupigiwa mfano na kuendelezwa,”- amesema Rais Samia.

Aidha amebainisha kuwa urafiki wa Tanzania na China umewezesha kujengwa kwa chuo hicho nakuokoa fedha nyingi ambazo zingetumika kuwapekeka wanafunzi nje ya nchi.

Pia ameeleza kuridhishwa na ujenzi wa jengo hilo nakuwataka wataalamu na uongozi wa chuo hicho kuhakikisha wanatumia majengo hayo vizuri katika kutanua wigo wa mitaala kwa washiriki kutoka ndani na nje ya nchi na kuleta tija kwa taifa.

Kwa Upande wake Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt.Stergomena Tax, ameshukuru Serikali ya China kwakuchangia Bilioni 57 katika Ujenzi wa mradi huo muhimu nakueleza namna itakavyosaidia kujenga taifa kwenye nyanja ya uongozi kwa vyombo vya usalama.

“Vyuo vya ulinzi wa Taifa ni muhimu katika Taifa kwani ni sehemu ambayo husaidia taifa katika kujenga ulinzi imara wa taifa ikiwa ni pamoja nakuwajengea uwezo viongozi wa Jeshi,”-amesema Waziri Tax.

Kwa Upande wake Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo amesema kukamilika kwa Mradi huo utasaidia kutoa mafunzo kwa Maafisa wa Jeshi wengi zaidi tofauti na ilivyokuwa hapo awali nakuongeza chachu ya maendeleo katika nyanja zote za kiuchumi na kijamii.

Naye Balozi wa China nchini Tanzania Chen Ming Juan amesema anaamini kuwa urafiki wa Tanzania na China ulioasisiwa na waasisi wa Mataifa hayo mawili unachangia kwa kiasi kikubwa katika masuala mbalimbali ya Maendeleo.

Miang amesisitiza kuendelezwa kwa mahusinao baina ya Mataifa hayo mawili kwani umekuwa na mchango katika masuala mbalimbali ya maendeleo ya Taifa la Tanzania hasa katika miradi mikubwa ya kimkakati ikiwemo reli ya Kisasa, Bwawa la Nyerere pamoja na kwenye sekta ya elimu hususani Jengo la Library ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam pamoja Jengo jipya ambalo hii leo lmekabidhiwa kwa Jeshi la Ulinzi wa Tanzania.

Zaidi ya Bilioni sitini zimeelezwa kutumika katika Ujenzi wa jengo hilo jipya ambapo Serikali ya China imechangia Bilioni 57 huku kiasi cha pesa kilichobaki kikichangiwa na Serikali ya Tanzania.