Tanzania imechaguliwa kuwa mjumbe
wa Baraza Kuu la
Shirika la Mawasiliano Duniani (ITU), baada ya kupata kura 141 kati ya 180 zilizopigwa huko Bucharest nchini Romania.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Nape Nnauye amesema, Tanzania imeshinda nafasi hiyo kutokana na dunia kutambua kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuimarisha Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) nchini.
Tanzania ilikuwa inawania ujumbe katika Baraza Kuu la ITU kwa kipindi cha mwaka 2023 hadi 2026, ambapo kulikuwa na wagombea 17 wa nafasi 13 za Afrika.
Baraza hilo linasimamia utekelezaji wa Sera, Mipango na Mikakati ya ukuzaji sekta ya Mawasiliano duniani, huku ajenda ya msingi ikiwa ni kuhakikisha wakazi wa sayari dunia wanaunganishwa na huduma za mawasiliano zenye uhakika na ubora.