Tanzania inatarajia kuanza kuuza nyama nchini Saudi Arabia baada ya nchi hiyo kufanya ukaguzi na kuridhishwa na maeneo mbalimbali yanayohusika na uchakataji wa mazao ya mifugo ikiwemo machinjio, maabara na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Prof. Elisante Ole Gabriel ambapo ameeleza kuwa baada ya ukaguzi ujumbe wa Saudi Arabia umetoa mapendekezo kadhaa ya kuboresha ili biashara hiyo iweze kufanyika kwa viwango vinavyohitajika.
“Haya masoko ya nje ya nchi ni mazuri kwa sababu yanatupatia fedha za kigeni lakini pia yanawahakikishia wafugaji wetu soko la uhakika kwa mazao ya mifugo yao,” amesema Prof. Ole Gabriel.
Aidha, Prof. Gabriel alitoa rai kwa wafugaji nchini kuchukulia hatua hiyo kama ni fursa kubwa na hivyo wahakikishe wanaboresha ufugaji wao kuwa wa kisasa zaidi ili kukidhi soko hilo la kimataifa.
“Serikali ni rahisi kutafuta masoko lakini je, mifugo iliyopo inakidhi soko hilo? hivyo niwaombe wafugaji na wafanyabiashara watumie fursa hii vizuri ili kuboresha uchumi wao na wa Taifa pia,” ameongeza Prof. Ole Gabriel.
Wizara imesema sekta ya mifugo kwa sasa inachangia pato la Taifa kwa asilimia 7.4 lakini lengo la wizara ni kufikia asilimia 15 ifikapo mwaka 2025 na hilo linawezekana kama milango ya masoko nje ya nchi ikianza kufunguka kwa uhakika.
Ikumbukwe hivi karibuni, Rais Samia Suluhu Hassan alikutana na Mwanamfalme wa Saudi Arabia ambapo miongoni mwa maeneo yaliyoangaliwa ni pamoja na sekta ya mifugo na aliielekeza wizara kutafuta masoko nje ya nchi ikiwemo nchi ya Saudi Arabia.