Tanzania kuongeza soko la mazao Uturuki

0
158

Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango amekutana na kufanya mazungumzo na Balozi wa Tanzania nchini Uturuki, Idd Seif Bakari, mazungumzo yaliofanyika jijini Dodoma.

Dkt. Mpango amemuagiza Balozi Idd Seif Bakari kuhakikisha anatekeleza diplomasia ya uchumi ikiwemo kutafuta masoko ya bidhaa zinazozalishwa Tanzania pamoja na kutafuta wawekezaji hususani katika maeneo ya kipaumbele.

Amemsihi kuendeleza na kukuza uhusiano baina ya Tanzania na Uturuki kwa manufaa ya pande zote mbili.

Makamu wa Rais pia amemtaka Balozi Bakari kuhakikisha anashiriki katika mikutano itakayowezesha kujifunza, kueleza mazuri ya Tanzania pamoja na kutangaza utalii.

Kwa upande wake Balozi Idd Seif Bakari ametaja fursa zinazotokana na ushirikiano baina ya Tanzania na Uturuki kuwa ni pamoja na kuuza mazao nchini Uturuki kama vile Pamba, Kahawa, Chai na Tumbaku.

Amesema kutokana na Uturuki kuendelea kwenye sekta ya viwanda vya nguo Ubalozi wa Tanzania nchini humo unatarajia kuongeza soko la mazao na kuhakikisha wawekezaji wa Uturuki wanawekeza Tanzania na kuongeza thamani ya mazao hapa hapa nchini.