Tanzania imeahidi kuendelea kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa (UNHCR) katika kutatua changamoto zinazotokana na uwepo wa wakimbizi nchini pamoja na kutafuta suluhu ya kudumu kwenye nchi zao ili Wakimbizi hao waweze kurejea makwao.
Ahadi hiyo imetolewa nchini Japan na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa wakati wa mazungumzo yake na Kamishna Mkuu wa UNHCR, – Filippo Grandi
kwenye kituo cha maonesho cha Yokohama baada ya kuhitimishwa kwa mkutano wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika (TICAD 7).
Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza umuhimu wa UNHCR kuisaidia mikoa inayokaliwa na Wakimbizi kutokana na mazingira yake kuharibiwa.
Kwa upande wake, Kamishna Mkuu huyo wa UNHCR, – Filippo Grandi
ameeleza kufurahishwa na utayari wa Tanzania katika kupokea Wakimbizi
na usikivu wa Rais John Magufuli katika kushughulikia changamoto za
Wakimbizi.
Waziri Mkuu Majaliwa yupo nchini Japan kumwakilisha Rais Magufuli kwenye mkutano huo wa kilele wa Saba wa Kimataifa wa Tokyo kuhusu Maendeleo ya Afrika ambao umehitimishwa hii leo.