Tanzania haina mgonjwa wa Ebola

0
179

Wizara ya Afya imesema kuwa hakuna mgonjwa wa Ebola aliyeripotiwa nchini.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Naibu waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel imewataka wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa huo, licha ya kuwa haujaingia nchini.

Tahadhari hiyo ni pamoja na kunawa mikono kwa maji safi na sabuni, kuepuka kugusa mwili au majimaji ya mwili wa mhisiwa au mgonjwa wa Ebola, na kuepuka safari zisizo za lazima kutembelea maeneo yaliyoathirika na ugonjwa huo.

Dkt. Mollel amewaagiza waganga wakuu wa mikoa na halmashauri nchini kuimarisha utoaji wa elimu, ufuatiliaji wa ugonjwa, uchunguzi wa kitaalam na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba.

“Nimewaagiza waganga wakuu wa mikoa na halmashauri nchini kuimarisha utoaji wa elimu, ufuatiliaji wa ugonjwa, uchunguzi wa kitaalam na kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba na kinga muhimu katika maeneo yao. Vilevile, nimewaelekeza kuimarisha uchunguzi wa wageni wanaoingia nchini kupitia mipaka yetu ikiwemo matumizi ya vipima joto (thermal scanners).” ameagiza Dkt. Mollel

Jana, Uganda ilitangaza mlipuko wa ugonjwa wa Ebola, baada ya watu sita kufariki dunia huku mgonjwa mmoja vipimo vya maabara vikithibitisha kuwa anaugua ugonjwa huo katika Wilaya ya Mubende iliyopo katikati ya nchi hiyo.