Tanzania, Burundi zakubaliana biashara mkongo wa mawasiliano

0
256

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Tanzania, Nape Nnauye, pamoja na viongozi na wadau wa mawasiliano, wameshuhudia utiaji saini mkataba wa makubaliano ya kibiashara kati ya Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) na Burundi Backbone System (BBS) katika hoteli ya Johari Rotana, Dar es Salaam.

Waziri Nape amesema tukio hilo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano wa kibiashara na kiteknolojia kati ya Tanzania na Burundi, na kufungua njia ya ushirikiano mpana zaidi katika sekta ya mawasiliano.

Mkataba huo mpya wa kibiashara kati ya TTCL na BBS una thamani ya dola za Marekani milioni 3.3, sawa na shilingi bilioni 8.3 za Tanzania.

Waziri Nape amebainisha kuwa matokeo mazuri ya huduma za Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano yamesababisha Serikali ya Burundi, kupitia BBS, kukubali kuongeza huduma hizo. Mkataba huo utaimarisha uhusiano wa kibiashara kati ya Tanzania na Burundi na kuboresha mawasiliano kati ya nchi hizo mbili.

Mkataba huo wa ushirikiano umesainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Peter Ulanga na Mkurugenzi Mkuu wa BBS, Jeremie Diomede Hageringwe.