Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) umewataka wananchi kutotupa taka hovyo na kutofanya biashara katika maeneo yaliyotengwa kwa shughuli mbalimbali ikiwemo waenda kwa miguu, ili kuepusha usumbufu na madhara yanayoweza kujitokea.
Wito huo umetolewa na Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Matengenezo TANROADS mkoa wa Dar es Salaam, Eliseus Mtenga wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye ziara ya ukaguzi wa matumizi ya fedha za kukarabati barabara zilizotolewa na Mfuko wa Barabara Tanzania.
Mtenga amesema kuwa kwa sasa kumekuwa na wafanyabiashaara hasa machinga wanaotumia eneo la waenda kwa miguu, na hivyo kuwalazimu wanaotembea kwa miguu kupita pembezoni mwa barabara kuu, hali inayoweza kusababisha ajali na kupelekea majeraha, ulemavu au kifo.
Aidha, amewaonya wale wote wanaotupa takataka kwenye mitaro ya maji taka kuacha mara moja kwani kuziba kwa mitaro hiyo kutasababisha mafuriko yanayohatarisha usalama wa raia, mali zao na miundombinu ya barabara.
Awali, Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, Joseph Haule ameiagiza TANROADS kufuatilia, kuwabaini na kuwachukulia hatua za kisheria wale wote waliounganisha mifumo yao ya maji taka kwenye mitaro ya barabarani vitendo ambavyo vinaweza kuababisha magonjwa mbalimbali kama vile kipindupindu.
Kwa upande wake mtendaji mkuu wa mfuko huo, Eliud Nyauhenga amesema mfuko huo umefanya kazi kubwa ya kutenga fedha kwa ajili ya kukarabati barabara mijini na vijijini, na kwamba katika mwaka wa fedha 2020/2021 walitumia zaidi ya bilioni 900 kufanikisha mpango huo katika maeneo mbalimbali nchini.