TANROADS kuanza ujenzi Daraja la Jangwani

0
179

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) unatarajia kuanza kutekeleza mradi wa kimkakati wa ujenzi wa Daraja la Jangwani mkoani Dar es Salaam ili kumaliza adha ambayo imekuwa ikiwakumba wananchi hasa nyakati za mvua.

Bashungwa ameyasema hayo bungeni jijini Dodoma wakati wa kuwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara yake kwa mwaka wa Fedha 2024/2025, ambapo amesema mradi huo ni sehemu ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa maendelezo ya Bonde la Mto Msimbazi.

Amesema daraja hilo litakalojengwa lina urefu wa mita 390 pamoja na barabara unganishi zenye urefu wa mita 710 na kina cha mita 15.5 kutoka usawa wa bahari.

“Daraja hili litakapokamilika litatatua changamoto ya kujaa kwa maji katika Barabara ya Morogoro eneo la Jangwani wakati mvua, na kusababisha kufungwa kwa barabara hiyo mara kwa mara,” ameongeza Bashungwa.

Amesema tathmini ya zabuni ili kumpata mkandarasi na mhandisi mshauri zinaendelea.