Mkuu wa wilaya ya Temeke mkoani Dar es salaam Godwin Gondwe amelipongeza Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kwa kufanikisha tamasha la Twenzetu kwa Yesu, na kusema matamasha kama hayo yanasaidia kuwaandaa vijana kuwa Wazazi na Viongozi bora.
Gondwe ametoa pogezi hizo mara baada ya kumalizika kwa tamasha hilo katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es salaam, tamasha lililoshirikisha Waimbaji mbalimbali wa Injili kutoka ndani na nje ya Tanzania
“Kanisa limefanya Jambo jema sana kuandaa tamasha hili, na mafundisho waliyoyapata hapa vijana yatasaidia kuzalisha Viongozi na Watanzania wanaoipenda nchi yao,” amesema Mkuu huyo wa wilaya ya Temeke.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Upendo Media Neng’ida Johannes amesema tamasha hilo limewasaidia vijana kujitambua na kuupongeza uongozi wa KKKT kwa maandalizi mazuri ya tamasha hilo.
Mmoja wa vijana walioshiriki tamasha hilo Anania Ndondolile ambaye pia ni Mwenyekiti wa vijana Dayosisi ya Mashariki na Pwani amesema kwake tamasha hilo limekuwa msaada mkubwa, kwani amejifunza namna ya kujiongoza katika maisha yake pamoja na namna ya kufanikiwa katika uongozi.
Tamasha la Twenzetu kwa Yesu limekuwa likifanyika Kila mwaka na kushirikisha dini na madhehebu mbalimbali na kauli mbiu ya tamasha hilo kwa mwaka huu ni you Are chosen (umechaguliwa).