Tamasha la Kimataifa la Utamaduni na Sanaa kufanyika Bagamoyo

0
220

Katibu Mkuu wa Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi, na Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Zainabu Abdallah, Oktoba 8, 2021 wamekagua maandalizi ya Tamasha la 40 la Kimataifa la Bagamoyo.

Tamasha hilo linatarajiwa kuanza Oktoba 28-30 mwaka huu na litahusu maonesho na utumbuizaji utakaoshirikisha wasanii wa sanaa mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo ngoma, uchoraji, uchongaji, maigizo, mitindo na muziki wa asili na wa kizazi kipya.

“Tamasha hili ni la kimataifa kwa hiyo mwaka huu tunakwenda kuliongezea zaidi fani mbalimbali; tunataka mwaka huu mtu aje Bagamoyo, alale Bagamoyo, ale Bagamoyo na ashuhudie urithi wa utamaduni na sanaa akiwa hapa Bagamoyo kwa siku zote tatu hadi nne hizo bila kutoka na kisha atembelee maeneo yetu ya kiutalii,” alisema Dkt. Abbasi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya aliyeambana na Katibu Tawala (DAS) Kasilda Mgeni, amesisitiza kuwa Mkoa wa Pwani na Bagamoyo wako tayari kuendelea kuwa wenyeji wa Tamasha hilo kuhakikisha Bagamoyo inaendelea kuwa kitovu cha utamaduni na sanaa hususani wakati huu ambapo Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Royal Tour, anaposisitiza muunganiko wa utamaduni wetu na utalii.