Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema matokeo ya sensa ni muhimu kwa mipango ya maendeleo.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa katika hafla ya ufunguzi wa usambazaji na mafunzo ya matumizi ya matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022 kwa viongozi na watendaji wa Mkoa wa Lindi, Nape amesema matokeo ya sensa ni msingi muhimu wa kufanya maamuzi sahihi katika sera na mipango ya maendeleo.
Amesema takwimu za sensa zinapaswa kuzingatiwa katika mipango yote ya maendeleo; iwe ni mipango ya muda mfupi, muda wa kati au muda mrefu.
Amesema kupitia takwimu za sensa maamuzi ya maendeleo yanapaswa kuzingatia idadi halisi ya watu, umri na viashiria vingine vya kidemografia.
Amesema, takwimu za sensa pia zinaweza kuonesha hali ya upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu, maji, barabara na umeme ambazo ni muhimu katika kupanga maendeleo ya wananchi.
Waziri Nape amesisitiza umuhimu wa mafunzo hayo katika kuimarisha uwezo wa watendaji katika kutumia takwimu za sensa. Watendaji hao wanaoshiriki mafunzo wanahusika katika kupanga mipango ya maendeleo ya jamii na hivyo mafunzo hayo yatasaidia katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.