TAKUKURU yawasimamisha kazi waliojenga nyumba zilizomkera Rais Magufuli

0
412

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imewasimamisha kazi watumishi tisa waliohusika katika usimamizi na ujenzi wa majengo saba ya ofisi za taasisi hiyo ambayo Rais John Magufuli alieleza kutoridhishwa na gharama za ujenzi wake.

Uamuzi huo umetolewa saa 24 baada ya Rais Magufuli kusema kuwa gharama za ujenzi wa nyumba hizo zilizojengwa katika wilaya saba hapa chini ni kubwa ikilighanishwa na nyumba zenyewe.

Akizundua moja ya nyumba hizo eneo la Chamwino, Dodoma, Rais Magufuli alielezea kutoridhishwa kwake na gharama kubwa zilizotumiwa na TAKUKURU, shilingi bilioni 1 sawa na wastani wa shilingi milioni 143 kwa kila nyumba, kwani majengo yaliyojengwa yana thamani ndogo ikilinganishwa na fedha zinazotajwa kutumia.

Rais Magufuli alimuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brig. Jen Mbungo kurekebisha dosari alizotaja kuwa zinaikabilia taasisi hiyo.

Aidha, alionesha kushangazwa na TAKUKURU kutaka kujenga ofisi ya taasisi hiyo katika Wilaya ya Chato kwa kuwa tayari wilaya hiyo inalo jengo la TAKUKURU alilolikabidhi yeye mwenyewe akiwa Waziri wa Ujenzi.