Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani Songwe, imeokoa nyumba yenye thamani ya shilingi milioni 165 iliyochukuliwa baada ya mmiliki kushindwa kurejesha mkopo wa shilingi milioni 15.
Nyumba hiyo iliyopo kwenye eneo la Mlowo wilayani Mbozi, ni mali ya Jacob Masebo ambaye alichukua mkopo huo kwa Richard Kalonge mwaka 2009.
Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Songwe, – Damas Suta amesema, Masebo alikopa shilingi milioni 15 miaka 11 iliyopita, ambapo alipaswa kurejesha shilingi milioni 33 ndani ya siku nane na endapo angeshindwa kutoa kiasi hicho cha fedha nyumba hiyo ingechukuliwa na Kalonge.
Amesema baada ya kupita siku hizo Masebo alishindwa kulipa fedha na hivyo nyumba yake yenye ghala kubwa moja, maghala madogo mawili na vyumba vitatu vya maduka ilibadilishwa hati na kuwa mali ya Kalonge.
Kamanda huyo wa TAKUKURU mkoa wa Songwe amesema jambo lililofanywa na Kalonge ni uonevu kupitia mikopo umiza, kwa kuwa baada ya kujimilikisha nyumba ya Masebo, alitumia hati hiyo kukopa shilingi milioni 70 benki ya CRDB.
Naye Mkuu wa wilaya Mbozi John Palingo ambaye amemkabidhi hati mpya Masebo, amewasihi Wananchi kuwa makini wanapofanya makubaliano yoyote kwa kuelewa vizuri mkataba ulivyo ili waepuke kuingia mikataba yenye makubaliano yenye utata.