TAKUKURU yaokoa bilioni 12 stendi mpya ya mabasi Dar

0
970

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kwa kushirikiana na Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Zipora Liana imeweza kudhibiti zaidi ya shilingi bilioni 12 ambazo zingeweza kulipwa kwa wakandarasi wanaojenga stendi mpya ya mabasi, Mbezi Luis, kama ziada kwa kazi ambayo haikufanywa.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam Mkurugenzi wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali John Mbungo amesema udhibiti huo umefanikiwa baada ya wachunguzi na wataalamu wa ujenzi kutoka taasisi hiyo kufuatilia ujenzi wa mradi huo kwa karibu.

Taarifa ya TAKUKURU imekuja ikiwa ni mwezi mmoja tangu Rais Dkt. John Magufuli alipoagiza mamlaka za Serikali kuhakikisha kuwa hakuna fedha za Serikali zitakazopotea katika ujenzi huo.

“Huu ni mwendelezo wa hatua nyinginezo ambayo taasisi hiyo imekuwa inazichukua katika kuthibiti vitendo vya rushwa nchini, sawa sawa na maelekezo ya Rais Dkt John Magufuli ya kuitaka taasisi hii kufutilia kwa karibu miradi ya maendeleo kwa minajili ya kuzuia na kupambana na vitendo vya rushwa,” amesema Mbungo.

Mbali na Dar es Salaam, TAKUKURU imefanikiwa kuokoa fedha za Serikali na za watu binafsi kutoka katika mikoa mbalimbali ikiwa ni mkakati wa mamlaka hiyo kudhibiti vitendo vya rushwa, wizi na ubadhirifu.

Mkoani Manyara wananchi wawili wamerejeshewa jumla ya shilingi milioni 33.2, huku mkoani Mbeya TAKUKURU ikiendelea na uchunguzi juu ya ujenzi wa Bwawa la Maji la Lwanyo ambalo inadaiwa limejengwa chini ya kiwango.

Bwawa hilo limegharimu shilingi bilioni 2.951 lakini kwa sasa halitumiki kama ilivyokusudiwa.